Friday, 6 July 2012

mgomo unaendelea muhimbili

Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakimpeleka Mgonjwa wodi ya Sewahaji jana baada ya kushindw akufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Mifupa (MOI) jana kutokana na mgomo wa madaktari. Picha na Juliana Malondo
Waandishi Wetu
WAKATI uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ukitangazia umma kwamba huduma katika taasisi hiyo zimerejea kama kawaida, uchunguzi wa kina wa Mwananchi umebaini kwamba huduma katika taasisi hiyo na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), bado zinasuasua.Juzi, uongozi wa MOI ulitoa taarifa kwa umma ukisema mgomo wa madaktari bingwa uliokuwa umetangazwa awali ulikwisha, huku uongozi wa MNH nao ukisema huduma zimerejea katika kiwango cha kati na kutaka wagonjwa waendelee na huduma kama kawaida.

Uchunguzi uliofanywa jana katika taasisi hiyo ya MOI na MNH na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, ulionyesha taarifa hizo mbili zinapingana na hali halisi ya utoaji huduma na mahudhurio ya wagonjwa katika hospitali hizo mbili.

Uchunguzi huo ulibaini kwamba, kitendo cha uongozi wa MOI kuwatembeza waandishi wa habari kujionea huduma za upasuaji juzi, kilikuwa ni mchezo wa kupanga ili kuonyesha umma kuwa huduma zimerejea.

Chanzo chetu cha habari kilisema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence Museru alifanya jukumu la kuwapigia simu madaktari ambao anawajua ili kumnusuru na adha hiyo ya mgomo wa madaktari.
“Mkurugenzi (Profesa Museru), aliwapigia simu madaktari akiwataka kufika kufanya upasuaji ili nyie waandishi mkipiga picha mwonyeshe kuwa huduma zimerejea,” kilisema.

Hata hivyo, alipoulizwa Profesa Maseru alijibu: "Hatuna sababu ya kudanganya mtu. Lakini, kama unataka maelezo zaidi naomba uje ofisini."

Juzi akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya MOI, Profesa Charles Mutalemwa alisema toka Jumatatu wiki hii madaktari 79 wamerejea kazini.

Profesa Mutalemwa alisema madaktari bingwa waliorejea ni 18 na 61 ni madaktari wa kawaida na walioko mafunzoni hivyo huduma zinaendelea kuimarika kadri siku zinavyoendelea.
Mwananchi lilifika katika kitengo hicho kujionea hali halisi ya huduma na kukuta wagonjwa wakipangiwa kufika hapo mwanzoni mwa mwezi ujao.

Kauli za wagonjwa
Aidan Kisanga ambaye alifika katika kliniki kutokana na tatizo la kuvunjika mguu, alisema, licha ya kutakiwa kuonana na dakatri jana, imeshindikana.
“Nimeambiwa nirejee hapa Juni 30 mwaka huu au kama nitasikia taarifa katika vyombo vya habari kuwa huduma imerejea. Inaniuma kwani mguu wangu unaniuma na sijui nitafanya nini,” alisema Kisanga.
Jakobo Chacha mkazi wa Kitunda, alisema alifika hospitalini hapo saa 11.30 asubuhi jana na kupewa namba 26, lakini hakupata matibabu baada ya mhudumu ambaye hakumfahamu, kuwatangazia kuwa hakuna huduma kutokana na ukosefu wa madaktari.

“Tulitangaziwa kuwa tuondoke na waliokwishalipia huduma wabaki. Wasiolipia tulikuwa tunapangiwa kila mtu na tarehe yake,” alisema Chacha na kuongeza:

"Jana (juzi), tumeambiwa madaktari wamerejea na kutakiwa kufika kupata huduma kumbe ilikuwa ni uongo, wanatuambia twende hospitali binafsi sasa kama sisi wa hali ya chini si tutakufa?" alihoji.
Ezekiel Mkandainda ambaye amelazwa katika wodi ya Sewahaji, MNH, alisema mgomo bado unaendelea na jambo hilo limefanya baadhi ya wagonjwa kufariki na wengine kuamua kuondoka kutokana na kukosekana madaktari.

“Mwandishi, madaktari bado wanaendelea na mgomo, leo (jana) ilikuwa siku yangu ya kuonana na daktari, lakini hatujamwona daktari yeyote aliyepita wodini kwetu zaidi ya wauguzi,” alisema na kuongeza:

“Wagonjwa wengi wameondolewa na ndugu zao kwenda kutibiwa kwenye hospitali za watu binafsi. Mimi nimetoka Mkoa wa Kigoma nina matatizo ya kibofu cha mkojo natakiwa nifanyiwe upasuaji, lakini hadi leo sijafanyiwa.”

Mgonjwa mwingine aliyelazwa katika wodi ya Mwaisela, MNH, Aisha Abdallah alisema wagonjwa waliopo katika wodi hiyo ni wachache kutokana na wengine kuondolewa na ndugu zao baada ya kukosekana madaktari.

Uongozi MNH
Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alisema kusuasua kwa huduma hizo kumetokana na madaktari hao kuanza kazi Julai 2 mwaka huu ambao ni wachache.
“Kuhusu huduma kusuasua ndiyo kwanza madaktari wameanza kazi wiki hii siku ya Jumatatu hivyo, tusitegemee huduma kuwa nzuri kama mwanzo. Madaktari watakapokuwa wengi huduma zitatolewa kama kawaida,” alisema Aligaesha.

KCMC, Mount Meru bado
Wakati huo huo, madaktari zaidi ya 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC waliondoka jana kwenda jijini Dar es Salaam na kusababisha huduma hospitalini hapo kuzorota.

Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea hospitali hiyo jana, alishuhudia idadi ndogo ya wagonjwa walioko wodini huku kliniki zote zikiwa zimesitisha utoaji huduma kutokana na mgomo huo.
Daktari mmoja bingwa aliyekutwa akitoa huduma, aliliambia gazeti hili kuwa, kwa sasa hawapokei wagonjwa wa rufaa wala kuendesha upasuaji wa kawaida isipokuwa upasuaji wa dharura tu.

“Uamuzi wa kuwarudisha resident doctors (wanaosomea ubingwa) kwa mkuu wa chuo haukuwa wa busara…,wewe unaona interns doctors hawapo halafu unawaondoa tena na resident,”alilalamika.
Madaktari wanaosomea ubingwa wako kati ya 50 na 60 hivyo ukichanganya na madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo, hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa madaktari karibu 140.

Taarifa zilidai kuwa, madaktari walioko katika mafunzo kwa vitendo wapatao 80 waliondoka mjini Moshi jana kwenda Dar es Salaam baada ya kutakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya leo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa KCMC, Dk Moshi Ntabaye ameshikilia msimamo wa kutotoa ushirikiano kwa wanahabari hata pale anapofuatwa ofisini au kupigiwa simu yake ya kiganjani.
Mount Meru warejea kazini

Hospitali ya Mkoa wa Arusha imesitisha zoezi la kuwaondoa madaktari 26 waliopo katika mafunzo kwa vitendo katika hospitali hiyo baada ya wote kusitisha mgomo baridi na kuendelea na kazi..

No comments:

Post a Comment