Wednesday 19 September 2012

KAMATI YA JUMUIA YA MADAKTARI YATOA TAMKO RASMI JUU YA UTEKELEZAJI WA MADAI YA MADAKTARI NCHINI

Kamati ya Jumuiya ya Madaktari Nchini , kwanza inapenda kutoa pole kwa Wanahabari wote nchini kwa kitendo cha kinyama ambacho Mwanaharakati na Mwandishi wa habari, Marehemu David Mwangosi alifanyiwa, hii ni ishara kuwa Jeshi la Polisi wameamua kutumia njia ya kuua raia ili kujenga hofu na woga miongoni mwa wapenda demokrasia na maendeleo nchini.


Pia tunapenda kulaani kitendo cha Serikali kupitia Wizara ya Michezo, Habari na Utamaduni kulifungia gezeti makini la Mwanahalisi kwa sababu ya kutoa taarifa za ukweli juu ya waliotaka kukatiza uhai wa Dr.Ulimboka Stephen, Jamii ya Madaktari na watanzania wengi bado wanaamini kuwa waliotajwa na gazeti la Mwanahalisi ni miongoni mwa waliohusika na kutekwa, kuteswa na kutelekezwa kwake na si yule anayesemekana kuwa na matatizo ya akili aliyedaiwa kukamatwa na Suleimani Kova. Hivyo tunalitaka Jeshi la Polisi litoe ripoti yake ya Uchunguzi ili kubaini ukweli wa taarifa hii.


Pia, tunachukua nafasi hii kupongeza mshikamano ambao Madaktari wameendelea kuuonyesha licha ya changamoto nyingi tunazopitia, ni vema ikafaamika kuwa ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa MAT na MAT imefunguliwa kesi 2 mahakamani, Ni katika kipindi hiki ambacho zaidi ya interns 300 wanasubiri kuitwa kuhojiwa na MCT bila kujua ni lini hilo litafanyika, Ni katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari anapata mapumziko baada ya kutoka katika Matibabu nchini Afrika Kusini, lakini ni katika kipindi hiki ambacho mpaka sasa hakuna hata hoja moja ya Madaktari imefanyiwa kazi na Serikali.


Tunapenda ieleweke kuwa suala la madai ya Madaktari si tukio, ni mchakato ambao utaendelea kwa vizazi vya sasa na vijavyo, ndio maana tumeshuhudia migomo hii katika nyakati tofauti pamoja na kujitokeza kikundi au mtu kutumiwa kuomba msamaha kwa lengo la kudhalilisha taaluma na kurudisha nyuma jitihada za kuboresha hali ya afya nchini na maslai ya watumishi kwa ujumla.


Kuhusu suala la interns, Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 10, Julai 2012, Baraza la Madaktari Nchini lilitoa taarifa kwa umma kuwa imesitisha leseni za muda kwa Madaktari waliochini ya mafunzo kwa vitendo, pia waliahidi kuwaita kwa nia ya kuwahoji mmoja mmoja pindi wakatapokamilisha uchunguzi wao, cha kushangaza ni kwamba miezi 2 sasa imepita bila hilo kufanyika.


Katika vikao mbalimbali ambavyo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, na Kaimu Katibu Mkuu wameshiriki, wamekuwa wakisisitiza kuwa hili lipo kisheria na interns wasuburi kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa. Hivyo tunapenda kutumia nafasi hii kuitaka MCT itekeleze kwa haraka majukumu yake kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa haki.


Hivyo basi Kamati ya Jumuiya ya Madaktari imejiandaa vya kutosha na taratibu za kisheria na itahakikisha inaweka wakili pale interns watakapoanza kuhojiwa kwa kuwa sheria inayounda MCT inatoa hiyo nafasi.


Mwisho kabisa tunapenda kutoa wito kwa interns kutumia hekima na busara katika kipindi hiki kigumu, waepuke kutumiwa na kikundi cha watu ambao wanatumika au wanajitumia kwa maslai ya kustarehesha watawala.


                           IMETOLEWA NA; KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA.

No comments:

Post a Comment