Monday 24 September 2012

WAGENI VIHIYO WANAAJIRIWA HOTELINI





BAADHI ya wafanyakazi wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali hususan barani Asia, wameendelea kuajiriwa katika nyadhifa tofauti za juu kwenye hoteli kubwa za kitalii jijini Dar es Salaam wakati hawana ujuzi wa taaluma ya kazi husika.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa wafanyakazi hao huletwa na ndugu zao wenye madaraka makubwa katika hoteli hizo bila kujali taaluma zao, na wakati mwingine hufanya kazi za kawaida ambazo kisheria zinatakiwa kufanywa na wafanyakazi wazawa.
Gazeti hili limenasa orodha ya wafanyakazi wa moja ya hoteli kubwa maarufu zilizopo eneo la Kunduchi, yenye wafanyakazi wa kigeni 29 ambao takriban wote ni raia wa India ukiacha watendaji wachache wa juu kabisa.
Taarifa kutoka ndani ya hoteli hiyo ni kwamba wafanyakazi hao wengi wao hawana ujuzi kabisa na kazi walizoajiriwa kufanya, hivyo baada ya kuingia hufundishwa na wale wachache wazawa ambao hata hivyo hawathaminiwi.
Ili kukwepa mkono wa sheria za nchi kuhusu wageni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania wazalendo, baadhi ya wafanyakazi hao wasio na ujuzi (vihiyo), wamekuwa wakitumia majina tofauti hotelini hapo badala ya yale yaliyoko kwenye pasi zao za kusafiria au nyaraka za Idara ya Uhamiaji.
Baadhi ya wafanyakazi wazalendo wa hotelini hapo, walilidokeza gazeti hili kuwa mchezo huo umekuwa ukifanywa kwa ushirikiano wa watendaji wasio waaminifu ndani ya Idara ya Uhamiaji na wamiliki wa hoteli hiyo.
“Tumelalamika sana juu ya mchezo huu unaotunyima ajira, maana kazi wanazofanya hawana ujuzi nazo, tunawafundisha sisi, lakini wanaajiriwa wao na kulipana mishahara mikubwa; watu wa Uhamiaji tukiwaambia wanakuja wanazungumza na wamiliki mambo yanaishia hapo na kama haitoshi wanatutaja majina kwa wamiliki tunafukuzwa kazi kwa kutoa siri za ofisi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao wazalendo.
Katika orodha ya wafanyakazi wa kigeni 29 wa hoteli hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake, kazi zilizoainishwa nyingi ni za kawaida kama ufundi, udaktari, umeneja stoo, uhasibu na nyinginezo ambazo kimsingi wako Watanzania wengi wenye ujuzi wa kuzifanya.
“Yaani hapa ukiingia humu ndani utashangaa kuona watu wanavyoweza kwenda kwao kuleta ndugu, wake, waume na jamaa zao na kuwajaza kazini kwenye vitengo nyeti wakati hawafanyi lolote. Tunaye Store Controller, lakini ukisoma kibali chake cha kazi anatambulishwa kama Operation Manager,” kilisema chanzo chetu.
Vile vile katika orodha hiyo yuko mfanyakazi mmoja anatajwa kama injinia, lakini wafanyakazi wenzake wanasema hajui lolote, hatua inayowafanya kuiomba serikali kuingilia kati kuzikagua hoteli hizo ili kubaini kama wahusika wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na vibali vyao.
Nafasi za juu ambazo zinashikiliwa na wafanyakazi wazalendo hotelini hapo ni mbili, moja ikiwa ya Meneja Rasilimali Watu, ambaye hata hivyo anatajwa kutokuwa na kauli kwani wafanyakazi wazalendo wanapomlalamikia hawapi majibu ya kujitosheleza akidai kuwa yeye analetewa wafanyakazi na wakubwa zake. Mwingine mwenye wadhifa mkubwa ni Meneja Ulinzi.
Juhudi za kuwatafuta wasemaji wa hoteli hiyo, waziri mwenye dhamana na kazi pamoja na Idara ya Uhamiaji zinaendelea kutokana na jana kuwa siku ya wikiendi na hivyo watendaji hao kuwa mapumzikoni.

CHANZO:TANZANIADAIMA

No comments:

Post a Comment