Thursday 20 September 2012

SOMA KISA HIKI CHA KWELI NA KUSISIMUA!

Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma
sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize,
inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa
ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi
na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi. Ilikuwa ni mwaka
1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui
ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni.
Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama siku
hizi. Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira,
nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato
cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira
zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa
nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na
niliitwa kwa usaili. Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule
ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya
Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe
basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia
kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa
Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa
kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.
Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono
mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye
hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni
bwana, anakula na kujifanya
kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli alisema
kwa kudhamiria hasa. Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema
ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake
kwenda
kituo cha polisi ili nishughulikiwe… … Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja
aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana
alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta
nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana. Alikuwa ni kijana mtu
mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia,
nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na
nilimsimulia.
Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati
nimeibiwa fedha zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa
napanga namna ya kurudi Dar, kama huko polisi ningeaminika. Kama mzaha
vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia huko Arusha
na nikirudi Dar
nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba
nikirudi Dar nimpelekee fedha zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini
kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu
kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko.
Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri
mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole.
Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo
la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili
litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari
yetu. Karibu na mji wa Same kwenye saa saba
usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na
kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria
tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa
wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana
na hapo kando kulikuwa na maiti wawili. Nilijua ni maiti kwa sababu
walikuwa wamefunikwa gubigubi.
Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa
kanga kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia,
ingawa sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka
kama mitatu. Kalikuwa kameumie kwenye paji la uso, lakini kalikuwa
hai. Bila shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari.
Machozi yalinitoka.
Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti
wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale katoto
kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali
kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu
ajali ile tu, hadi tunafika
Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano
asubuhi, badala ya saa mbili . Nililala kwenye hoteli rahisi na
kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua
gazeti ambapo
nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye
ajali ile ya Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe.
Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina
lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi
Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.
Nillishindwa kujua ni kwa nini
afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali
yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga pia. Nilijua kwamba
nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi
tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa. Kwa mara ya
kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini nakuamua
kunipa fedha zile. Sikupata jibu. Nilikata kipande
kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa
kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi
deni la watu? Nilijikuta
nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule
mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la
marehemu kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili
nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku
hiyo hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili
ule kuwa mbaya
kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu
mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo
kupata nafasi ya
kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na hatimaye
nilibahatika kwenda nchini Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli
zangu. Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa
jengo Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na
kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu
niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa
anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui.
Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni
kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo.
Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya
yake ikiwa hairidhishi sana. Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani
niliona atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba
sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu
wenye
pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na ukifanya
haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi”. Nilisema na
sikuwa na kikao chochote , lakini nilitaka tu aondoke haraka.
“Samahani mzee, nilikuwa
na shida…..nimefuk uzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu
…..nime….niko ….kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea
mtu…….. Nilimkatisha. “Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la
kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua
kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu!
Nenda Wizara ya Elimu waambie…… Kwanza wazazi wako wanafanya kitu
gani,
kwa nini washindwe …..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana
uwezo, wanataka sifa?” “Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule
ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule.
Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye
ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi….,” Alianza kulia. Huruma
fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi, kwa nini
nisiwe mwema, angalau
kwa mara moja tu. “Baba na mama walifariki lini?” Niliuliza nikijua
kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni
ya ukimwi ilipoanza, ambapo kula anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa
ukimwi. “Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka
mitatu.
Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa
kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji
unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko
nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua. Kitu fulani
kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana. “Kwa nini
umeamua kuja kwangu, ni nani
alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?” Yule
kijana alisema, “Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza
kunisaidia, na ndionimejikuta nikiingia hapa, sijui……..sikutu mwa na
mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka1979  huko Same na mimi wanasema
nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa.” Alishika kwenye
kovu juu ya paji lake la uso.
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama vile
nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa nani?”
“Alikuwa anaitwa Siame….Cosmas Siame….” Niliinuka ghafla hadi yule
kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na
kuchafua kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka,
nilitoa kipande cha gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa
nimekihifadhi. “Ndio alikuwa anaitwa Cosmas
Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona.
Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. “Mungu, wewe ni mweza na hakuna
kinachokushinda . Nimeamini baba kwamba kila jema tunalofanya ni akiba
yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani.” Halafu nillinyamaza
na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa
binadamu kwa kila analofanya. Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa.
Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa. Nilimfuata yule kijana na
kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. “Mimi ni baba yako mdogo, ndiye
nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi mwisho” Naye alilia
bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiw a kabisa. Nilirudi kwenye
kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita. Tuliondoka hapo na
kwenda kumwona shangazi yake
Ubungo, eneo la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na
hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo
dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa
nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja baadae, lakini akiwa
ameridhika sana. Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi
sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi. Ukweli ni kwamba ni
mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake
wanafurahia kile walichokipanda miaka mingisana nyuma. Lakini nami
najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza
ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame hadi ofisini kwangu akizipita
ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu,
kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu…………
*************MW ISHO***********
Daniel Chongolo,
Ulimboka Street,
Mabwepande Area,
Kinondoni North west,
P.O.Box 9112,
D'Salaam.

1 comment:

  1. haleluyajah,hakika Mungu nimwema saana na anatenda mujiza na anaweza yoote jamani tusimpuuzie,pia kusadia nikitu kikubwa nakizuri kwetu sisi wanadamu kwani huwezijua kesho,kama ulivyoelezea hapo mdau nimeguswa saana na habari hii.ubarikiwe saana kaka.pia na kaka issackin.

    ReplyDelete