Monday 10 September 2012

USAFIRI WA RELI DAR KUANZA OCTOBER




USAFIRI wa reli kwa wakazi wa Dar es Salaam utazinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu kama ilivyopangwa, hata kama baadhi ya miundombinu itakuwa haijakamilika.Akizungumza ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Mohamed Mohamed alisema hadi sasa kila kitu kinakwenda  vizuri ingawa wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Mohamed alisema tayari kandarasi zimetolewa kwa kampuni tofauti kwa ajili ya ujenzi wa vituo na sehemu za kukatia tiketi, uwekaji kokoto katika reli, vifusi kwa baadhi ya maeneo, alama za tahadhari katika makutano ya barabara na umeme na vyoo.
“Kuna kampuni tumezipa kazi na nyingine tutazipatia kandarasi za huduma hizo, ili kufanikisha utekelezaji mradi huo ambao utahusisha kilomita 197 za reli,” alisema.
Alisema bajeti imeongezeka kutokana na kuibuka kwa changamoto ambazo utekelezaji wake unahitaji fedha, huku TRL ikiwataka waliopo ndani ya mita 15 kutoka ilipo reli, kuondoka ili kupisha utekelezaji mradi.
“Kuwapo ndani la eneo la hifadhi ya reli ni kosa kisheria, hivyo waliojenga maeneo hayo wanatakiwa kuhama haraka iwezekanavyo badala ya kusubiri kuchukuliwa hatua,” alisema Mohamed.
Mohamed alisema wamewasiliana na manispaa za Ilala na Kinondoni kuhusiana na wakazi waliopo makutano ya reli na barabara, ambao wanatakiwa kuwa umbali mita 92  ili ziangalie jinsi ya kuwaondoa kabla ya kuzinduliwa mradi.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment