Tuesday, 18 September 2012

Madaktari waomba radhi kwa madhara ya mgomo

*Wajutia mgomo wao uliofanyika hivi karibuni
*Wasema hawapo tayari kushiriki tena mgomo
MADAKTARI wanaofanya kazi chini ya usimamizi wa madaktari bingwa (Interns), wameomba radhi kwa wananchi na Serikali kutokana na madhara ya mgomo wao uliofanyika hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Walioathirika na Mgomo, Paul Swakala, alikiri kuwa mgomo huo umesababisha madhara makubwa.

Swakala alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa chama chake pia kinakusudia kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete, kwa lengo la kumwomba radhi.

“Tunatumia fursa hii kupitia kwenu waandishi wa habari kuwaomba radhi Watanzania wote na kwa Serikali kutokana na madhara yaliyosababishwa na migomo ile ambayo ushiriki wetu ulikuwa hauepukiki.

“Tunajua kuwa wapo watu walioathirika na mgomo ule, hivyo tunawaomba radhi kwa Watanzania wote walioathirika na mgomo, pia kwa usumbufu uliojitokeza.

“Pamoja na kwamba utamaduni wa kuomba radhi hadharani kwa nchi yetu haujazoeleka, lakini tumeamua kufanya hivyo kwa sababu sisi ni binadamu na watu wote tuna upungufu.

“Pia tunamwomba radhi Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake kwa usumbufu uliosababishwa na mgomo ule, vile vile tunatambua na kuunga mkono juhudi zake katika kuboresha huduma za afya nchini pamoja na changamoto nyingi ambazo zinaikabili sekta hiyo nchini.

“Hata hivyo, tutazidi kuiomba Serikali iangalie zaidi sekta hii, kwani maisha ya Watanzania wengi yanategemea huduma bora za sekta hiyo.

“Tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa sisi vijana wao hatupo tayari tena kushiriki kwa namna yoyote katika migomo inayoweka rehani maisha ya Watanzania wenzetu,” alisema.

Swakala alisema kuwa madaktari wanajutia sana kosa hilo na wako tayari kurejea kazini kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa moyo wote.

Mtanzania

No comments:

Post a Comment