Tuesday, 30 October 2012

Dar waanza kutumia usafiri wa treni


 
Abiria  kutoka  Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam,  wakitumia usafiri wa treni ya Kampuni ya Reli Tanzania( TRL), jana asubuhi,  baada ya kuanza rasmi kwa safari kati ya maeneo hayo ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa jiji. Picha na Emmanuel Herman  

USAFIRI wa treni katika Mkoa wa Dar es Salaam umeanza rasmi jana ukitoa huduma hiyo kwa wakazi wake kuanzia Pugu Mwakanga hadi Kurasini na Ubungo Maziwa hadi Stesheni.
Huduma hiyo ambayo itakuwa ikipatikana kila siku asubuhi na jioni, inatolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).Usafiri huo ulianza saa 12.00 asubuhi kwa ile ya TRL ikitokea Ubungo Maziwa na kuwasili Posta saa 12.30. Abiria wa Pugu Mwakanga walisafiri katika treni ya Tazara saa 12.30 asubuhi na kufika Kurasini saa 1.00.
Katika uzinduzi huo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipanda treni za mashirika hayo yote mawili.Baada ya kuwasili Stesheni, treni hiyo ya TRL ilianza tena safari ya kuelekea Ubungo Maziwa saa 2:45 na iliwasili saa 3:10.
Hata hivyo, katika safari hizo za asubuhi, idadi ya abiria haikuwa kubwa ikielezwa kuwa ni kutokana na wengi wao kutokuwa na taarifa za kutosha za kuanza kwake na jinsi inavyopatikana huduma hiyo.
Katika baadhi ya maeneo, wananchi hata wale waliokuwa katika vituo vya mabasi, walionekana kushangaa na kuulizana.
TRL itatoa huduma hiyo ya usafiri wa reli kwa kutumia treni mbili zenye mabehewa sita yenye uwezo wa kuchukua abiria 80 wakiwa wameketi kila moja hivyo kuwa na uwezo wa kubeba abiria 480 kwa safari moja jambo ambalo linatarajiwa kupunguza msongamano wa abiria na magari  asubuhi na jioni.
Kwa upande wa Tazara, huduma hiyo itatolewa na treni moja yenye mabehewa sita ambayo ni kutoka Pugu Mwakanga kuelekea Kurasini Shimo la Udongo.
Akizungumza jana, Dk Mwakyembe alisema treni hizo zitafanya kazi kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi na kupumzika Jumapili ili kufanya matengenezo.
Kwa wasafiri wa kutoka Ubungo Maziwa mpaka Stesheni, kutakuwa na vituo vinane ambavyo ni Ubungo, Mabibo, Mwananchi, Matumbi, Buguruni Kwa Mnyamani, Tazara, Kituo cha Polisi Ilala, Kamata hadi Stesheni.
Kwa abiria wa Tazara, usafiri huo utaanzia Pugu Mwakanga na kusimama katika vituo vya Pugu, Lumo, Kigilagila, Kwa Alimboa, Kitunda, Moshi Bar, Kipunguni na Magnus Sekondari.Nauli kwa usafiri huo ni Sh400 kwa watu wazima na watoto na wanafunzi ambao watakuwa na behewa lao maalumu watalipa Sh100.
Kutokana na hali ya hewa katika Mkoa wa Dar es Salaam, mabehewa ya treni hizo yamefungwa pangaboi na redio.
Dk Mwakyembe alisema Serikali imetumia Sh2.36 bilioni kwa ajili ya kufufua njia za treni na mabehewa yake kiasi ambacho alisema ni kidogo ikilinganishwa na gharama za kukodi.
Akitoa mchanganuo wa fedha hizo, Waziri Mwakyembe alisema Sh2.1 bilioni zilitumika kwa ajili ya kufufua mabehewa 14 na Sh2.6 milioni kwa ajili ya kufanyia marekebisho njia yake.Alisema hatua hiyo imeokoa fedha za Serikali kwani kama ingeamua kukodi, ingeweza kutumia hadi Sh3 milioni kwa siku kwa kichwa kimoja.
“Nitahakikisha treni hii inafanya kazi katika kipindi chote nitakachokaa madarakani, nitasimamia kwa umakini.”
Changamoto zilizojitokeza
Licha ya treni hizo kuanza kazi, bado kazi ya matengenezo hasa ya vituo vya kupandishia abiria na vibanda vya tiketi havijakamilika kwani kilichoonekana kukaribia kuanza kutumika ni kimoja tu cha Ubungo.Aidha, eneo la kupishana treni za TRL Buguruni nalo lilikuwa halijakamilika na kutokana na hali hiyo, treni moja ilishindwa kufanya kazi jana.Pia ahadi ya Dk Mwakyembe ya maegesho ya magari katika eneo la Ubungo Maziwa haijatekelezwa kwani hadi jana hapakuwa na eneo lolote lililokuwa limetengwa kwa ajili hiyo. Waziri huyo alikuwa ameahidi kuwapo kwa eneo kubwa la maegesho kwa wakazi wenye usafiri ambao wangependa kutumia treni kuingia katikati ya jiji.
Abiria waduwaaAbiria wengi hawakuwa na taarifa za kutosha kuhusu kuanza kwa usafiri huo jana kiasi kwamba wengi wao walionekana wakipigwa butwaa kila treni hizo zilipopita.
“Hatujui kama treni imeanza safari leo, hii inatokana na kutosikiliza vyombo vya habari, jambo ambalo limesababisha wengi tung’ang’anie kwenye vituo vya daladala,” alisema Juma Omary (40) Mkazi wa Mabibo.
Aliitaka Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuanzishwa kwa usafiri huo ili waweze kuutumia kwa ajili ya shughuli zao.
Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Amina Jafari (43), alipongeza hatua ya Serikali kuanzisha usafiri huo akisema utapunguza msongamano wa abiria kwenye vituo vya mabasi na barabarani.
Aliitaka kuzingatia ahadi yake ya kutenga maeneo maalumu ya maegesho ili wananchi wengi zaidi watumie usafiri huo kuingia na kutoka katikati ya jiji badala ya magari binafsi.

Mwakyembe atoa angalizo
Dk Mwakyembe alitoa angalizo kwa wananchi watakaokuwa wakitumia usafiri huo kuzingatia muda akisema kinyume chake wanaweza kusababisha hatari au usumbufu.Aliwataka wananchi na vyombo vingine vya usafiri hasa pikipiki kuwa makini katika maeneo ambayo treni zinapita ili kuepusha ajali.

No comments:

Post a Comment