Tuesday 23 October 2012
MIL. 700 ZILIZOFICHWA KWA MRAMBA ZIKAIBWA, ZAZUA UTATA
UTATA umegubika kuhusiana na kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni shilingi milioni 700,000,000 zilizofichwa na Mary Mramba katika kabati nyumbani kwake Stakishari eneo la Sabasaba, Ilala jijini Dar es Salaam.
Fumuafumua ambayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu sakata la fedha hizo ambazo zilifichwa kati ya Novemba mwaka jana na Januari mwaka huu, imegundua kwamba ziliibwa na watu kadhaa wakiwemo ndugu zake.
Imegundulika pia kuwa Mary alitoa taarifa Kituo cha Polisi Stakishari Septemba mwaka huu na kufunguliwa jalada la kesi STK/RB/16109/2012 na jalada la upelelezi STK/IR/12865/2012 akimtuhumu mtoto wa kaka yake aitwaye Digna Mark na wenzake kuhusiana na kesi ya kughushi hati ya nyumba na wizi huo.
Uchunguzi wa Fumuafumua umebaini kwamba mara baada ya Mary kugundua mwezi Januari kuwa fedha hizo zilikuwa zimeibwa, hakutaka kupeleka suala hilo polisi kwa sababu anazozijua yeye bali alifanya kikao na wanandugu akiwemo Digna na kubaini tayari magari matano na nyumba mbili zilizokuwa zinamilikiwa na mtu huyo ni vitu vilivyokuwa vimenunuliwa kwa fedha hizo.
Alichokifanya Mary ni kumpigia magoti Digna arejeshee hayo magari na nyumba hizo kwani hakutaka suala hilo alifikishe polisi. Pia inasemekana hata ndugu zake wengine walitoroka na zaidi ya shilingi milioni 400 kati ya fedha zilizoibwa.
Imegundulika kuwa Digna aliiba shilingi milioni 300 na zingine ziliibwa na ndugu zake na kutoweka nazo.
Mlalamikaji hakuwashitaki watu hao bali alikaa kimya ikidaiwa kwamba angeshitaki angeulizwa alikozitoa fedha hizo nyingi.
Imebainika kwamba wanandugu hao waliamua kuiba fedha hizo wakiamini Mary asingeweza kuwashitaki kutokana na kwamba wanajua jinsi fedha hizo zilivyopatikana hivyo alihofia kuwa siri ingevuja.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba Mary aliamua mambo hayo yaishe kwa siri ndani ya familia badala ya kupelekwa polisi ambapo yaliisha kwa upande wa Digna kwani aliamua kurejesha mali alizonunua na fedha hizo alizochukua ambazo ni shilingi milioni 300.
Hata hivyo, Mary alilazimika Septemba mwaka huu kwenda polisi baada ya kusikia kwamba Digna ameenda huko kutoa taarifa kwamba hati ya nyumba yake ilikuwa imepotea.
Fumuafumua imegundua kuwa maelezo yaliyotolewa na Mary huko polisi juu ya fedha hizo ni kuwa alitumiwa na ndugu yake aitwaye Philipo Sindana aishiye nchini Italia kwa ajili ya kununua nyumba, kitendo kinachopingwa na Digna ingawa hajawa tayari kuelezea ukweli kwa sasa.
Hata hivyo, jalada la kesi hiyo liko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili iandaliwe hati ya mashtaka. Wakati jalada hilo halijarudi, polisi imeelezwa kwamba askari wa kituo hicho cha Stakishari walikuwa wakilaumiana kwamba maelezo yalioandikwa hayakutosheleza na kuna kitu kinafichwa.
Fumuafumua imebaini kwamba jalada hilo limesharudishwa toka kwa mwanasheria na kumweleza mkuu wa upelelezi Wilaya ya Ukonga, Idd Kiogomo kwamba hamna kesi ya kumshtaki Digna juu ya wizi ama kughushi bali ni kutoa taarifa za uongo za kupotelewa kwa hati ya nyumba.
Mkuu huyo wa upelelezi ameagizwa kutoa taarifa ya kina juu ya shitaka la wizi kwani maelezo ya Mary yanaonyesha kwamba wizi ulifanyika Januari hivyo iweje atoe taarifa hizo Septemba.
Kiogomo ametakiwa kuchunguza na kutoa maelezo juu ya upatikanaji wa fedha hizo nyingi na kwa nini zilihifadhiwa ndani. Vilevile Mary aeleze ni mahakama gani ilimpa kibali cha kutaifisha nyumba na magari ya Digna.
Itaendelea wiki ijayo ikiwa na maelezo ya Mary, mumewe na jeshi la polisi.
Chanzo:www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment