Saturday 20 October 2012

ASKARI FFU AUWAWA ZANZIBAR

POLISI YAWATUHUMU UAMSHO, YATANGAZA KUWASAKA POPOTE, VURUGU ZAENDELEA 
Na: Salma Said,MWANANCHI
MACHAFUKO yanayoambatana na ghasia, yamechukua sura mpya, baada ya askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), CPL Said Abdulrahman kuuawa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kikundi cha Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki). 
 Tukio hilo limekuja ikiwa ni siku moja baada ya kikundi cha watu hao kufanya ghasia wakitaka kiongozi wao, Sheikh Farid Hadi Ahmed aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha arudishwe wakiamini kuwa, polisi walimteka. Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa mauaji hayo yalifanyika eneo la Bububu katika mji wa Unguja Visiwani Zanzibar. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema Mjini Unguja jana kuwa, askari aliyeuawa ni mwenye namba F.2105 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), cha Mkoa wa Mjini Magharibi. "Wafuasi wa Uamsho wamempiga mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kutoka kazini saa 6:30 usiku eneo la Bububu.
 Tuelewe kwamba aliyeuawa ni askari polisi, ni raia wa Tanzania na ni muumini wa dini ni lazima tuhakikishe waliofanya unyama huu wanakamatwa," alisema na kuongeza: "Tutawasaka kwa udi na uvumba na kufikishwa mahakamani kwa mauaji na sheria za nchi zitachukua mkondo wake,” alisisitiza Kamishna huyo. Vurugu zaendelea Pamoja na tamko hilo, hadi jana jioni vurugu hizo ziliendelea kwa vijana hao kuchukua misalaba makaburini, viti na meza na kuviweka barabarani kisha kuvichoma moto.
 Mwandishi wa habari hizi na wenzake kadhaa, walinusurika kuvamiwa na wafuasi wa Uamsho wakati wanatokea eneo la Kwerekwe, baada ya kundi la watu kuwazunguka na kuziba barabara kwa magogo, kisha kuchoma matairi ya gari. 
"Tumefukuzwa kwa mawe na hao ubayaubaya na nusura niligonge gari. Jamaa walituzunguka katikati, wametuwekea magogo na huku wametuwashia matairi ili tusipite. Kidogo leo tufe billahi!" alisema mwandishi huyo. 
Kutokana na vurugu hizo, polisi iliwaita viongozi watano wa Uamsho na kuhojiana nao kuhusu suala hilo, na hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa na taarifa zaidi kuhusu hali hiyo. 
Akizungumzia tukio la kutoweka kwa kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed, Kamishna alisema: "Ilikuwa saa 6:30 mchana wa juzi tulipokea taarifa kutoka kwa Sheikh Msellem Ally kwamba kiongozi mwenzao wa Jumuiya ya Uamsho ametekwa na haonekani tangu jioni ya Oktoba 16. "Baada ya taarifa hii, uchunguzi ulianza na mmoja wa watu waliohojiwa ni Said Omar Said ambaye ni ndugu wa Sheikh Farid ambaye ni dereva na ndiye aliyekuwa naye walipokwenda katika eneo la Mazizini kununua umeme kutokana na maelezo ya dereva huyo." 
Kamishna Mussa alisema kwa mujibu wa Said, Sheikh Farid alimwamuru dereva huyo kwenda nyumbani kupeleka umeme wakati yeye akizungumza na watu walikuwamo ndani ya gari aina ya Noah ambalo hata hivyo nambari zake za usajili hazikufahamika. Alisema ilipotimu saa 6:30 mchana juzi wakati taarifa hizo zinapelekwa kituoni, wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho walikuwa wanaendelea kujikusanya katika msikiti wa Mbuyuni na kuanzisha fujo kwa kuwasha moto kwenye jaa lililokuwa karibu na msikiti huo. 
"Baadaye fujo hizo zilisambaa katika maeneo mengine ya mjini kwa kufanyika uharibifu wa mali za Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa kawaida,” alisema. Alisema katika vurugu hizo watu hao walichoma moto magari kadhaa, ambapo gari la Serikali lilivunjwa kioo kidogo cha pembeni, gari la Zimamoto kuvunjwa kioo cha mbele pamoja kuvunja duka la pombe na kuiba mali zilizokuwamo ndani. 
Kamishna Mussa alisema, mpaka sasa, watu 10 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo. Kauli ya SMZ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, SMZ, imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa maelezo kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya Zanzibar. Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu. 
Akizungumzia tukio la vurugu zilizotokea juzi, Aboud alisema kwamba vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid vilifanya vurugu katika mitaa ya Darajani, Michenzani, Mwembeladu, Magomeni na Amani wakidai kwamba kiongozi wao ametekwa. Alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya dola wakiwamo Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, KMKM, JKU, Chuo cha Mafunzo, Zimamoto na Valantia na vyote vimeeleza kuwa havielewi chochote kuhusu Sheikh Farid.
 Aboud alisema wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wao, wananchi wanapaswa kutulia na kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao. 
 Waziri Aboud alisema kuwa Serikali inawasihi wananchi kuacha kujiingiza katika fujo na vurugu kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitavumilia vitendo hivyo. 
CCM, CUF walaani Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa CCM, wamelaani ghasia zilizofanywa na kikundi cha Uamsho katika mitaa mbalimbali juzi. 
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa CCM kwenye Ukumbi wa Baraza hilo lililopo Bweni, Hamza Hassan Juma alisema wakati umefika kwa hatua kali za kisheria kuchukuliwa kabla ya hali haijawa mbaya zaidi. "Isifike mahali Zanzibar ikageuka taifa la machafuko na kuwafanya wananchi kushindwa kuishi kwa amani," alisema huku akimtaka Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema kusimama kidete kumaliza hali hiyo. Wawakilishi hao wa CCM, waliitaka Serikali kuwalipa fidia wote walioathirika na ghasia hizo na vikosi vya usalama SMZ kusaidia kuweka ulinzi wakati wote katika mji wa Zanzibar. 
Juma alifika mbali zaidi na kusema kuwa, Jumiki si chama cha siasa, hivyo kuiomba Serikali kuifuta kwa maelezo kwamba imekosa mwelekeo kwa kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani. Wajumbe hao waligoma kuingia Barazani jana ikiwa ishara ya kuonyesha msimamo wao kulaani hali hiyo. 
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi CUF kimeelezea kusikitishwa na matukio ya vurugu Visiwani Zanzibar. "Kutokana na vitendo hivyo, Chama cha Wananchi kinalaani kwa nguvu zote matukio hayo ambayo yamesababisha uvunjifu wa amani, na kusababisha hofu na taharuki kwa raia pamoja na wageni wanaotembelea Zanzibar”, ilisema taarifa ya CUF iliyotolewa Zanzibar jana. 
CUF katika taarifa hiyo, pia walieleza kushtushwa na habari za kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed katika mazingira ya kutatanisha, hivyo kuitaka SMZ kuzidisha juhudi za kumtafuta. 
Kwa upande mwingine, CUF inawataka wanachama wake, wapenzi na wananchi wote kutojiingiza na kutofanya vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani ya nchi yetu.

No comments:

Post a Comment