Tuesday, 23 October 2012

Viongozi wa Uamsho, mahakamani Zanzibar



                                                             Vurugu kisiwani Zanzibar
Viongozi saba wa kundi la kiislamu la Uamsho leo wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe huko kisiwani Zanzibar.
Mbele ya hakimu mkaazi wa mahakama hiyo, viongozi hao wameshtakiwa kwa kosa la kusababisha vurugu miezi miwili iliyopita.
Miongoni mwa masheikh waliopelekwa katika mahakama ya Mwanakwerekwe iliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Suleiman, Mselem Ali Mselem, Musa juma Issa , Suleiman Majisu pamoja na Haji Sadifa ambaye ni mkuu wa usalama wa Uamsho.
Wakiwa kizimbani, viongozi hao wamesomewa shtaka lao la kusababisha vurugu visiwani humo tarehe 17 na 18 mwezi Agosti mwaka huu.
Mwandishi wa BBC Abubakar Famau anasema kuwa wote kwa pamoja wamelikana shtaka hilo. Musa ali Musa ambaye ni Kamishna polisi Zanzibar amesema viongozi hao pia wamekabiliwa na mashtaka ya nyuma kwa sababu makosa ya jinai hayaozi.
Naye wakili wa washtakiwa hao aliiomba mahakama iwape dhamana wateja wake kwa madai kwamba kosa linalowakabili haliwazuii wao kupata dhamana. Wakili huyo amekwenda mbele zaidi kwa kuomba masharti nafuu ya dhamana.
Hata hivyo, hakimu wa wilaya ameahidi kulifikiria ombi hilo kesho kutwa pindi kesi itakaposikilizwa tena.
Hatua ya kukamatwa kwa sheikh Farid na wenzake inakuja siku kadhaa baada ya sheikh huyo kuripotiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana, hali iliyozua taharuki kubwa miongoni mwa wafuasi wake ambapo jeshi la polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Baada ya siku tatu za kutoweka kwake, taarifa za kuonekana kwa Sheikh Farid zilianza kuzagaa mwishoni mwa juma katika majira ya saa nne usiku. Hali iliyosababisha kiwewe ghafla na kuuamsha mji wa Zanzibar.
Licha ya kiongozi huo kudai kwamba alitekwa na watu wa usalama, lakini jeshi la polisi linaendelea kuikana taarifa hiyo.
Siku iliyofuatia, Sheikh alitakiwa kutoa taarifa yeye na wenzake katika kituo cha polisi ambapo walifanyiwa mahojiano yaliyodumu kwa zaidi ya saa tano na hatimaye kufunguliwa mashtaka.
Hivyo kufikishwa kwao mahakamani leo, wengi wamedhani ni kwa kosa la vurugu zilizotokea wiki iliyopita, hali iliyowaacha wengi na butwaa.
Vurugu zinazotokea mara kwa mara visiwani Zanzibar zinaonekana kuathiri shughuli za kiuchumi ikiwemo ile ya utalii. Kwa mujibu wa wafanyakazi wa sekta ya uchumi, tayari hali hii imepelekea wageni wengi kusitisha safari zao kwa kuhofia usalama wao.

bbcswahili

No comments:

Post a Comment