Tuesday 23 October 2012

Liundwe jeshi maalumu kulinda mbuga za wanyama



Monday, 22 October 2012 21:02

HABARI za maofisa wa forodha wa Hong Kong, nchini China kukamata kontena mbili za pembe za ndovu zinazodaiwa kutokea Tanzania na Kenya bila shaka zitakuwa zimewashtua na kuwakasirisha watu wengi hapa nchini. Pembe hizo zenye thamani ya Sh5.4 bilioni zilikuwa na vipande 1,209 vyenye uzito wa tani nne na zilikamatwa nchini humo siku tatu zilizopita zikiwa zimewekwa alama za kuonyesha kwamba zilikuwa zimebeba plastiki chakavu na maharage aina ya roscoco.

 Tukio hilo linasemekana limewaacha midomo wazi maofisa hao wa forodha nchini humo, kwani ni mara ya kwanza kwao kukamata kiasi kikubwa kama hicho katika historia ya nchi hiyo. Kugundulika kwa pembe hizo kumeelezwa kulitokana na taarifa zilizotolewa na maafisa wa Serikali ya China kwa maofisa wa forodha wa Hong Kong kuhusiana na pembe hizo.
Ni tukio ambalo pia limeishtua Serikali ya Tanzania, ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya walishtuka kusikia kuwapo kwa tukio hilo la kukamatwa kwa shehena kubwa ya pembe za ndovu kutoka Tanzania na Kenya na kusema watachukua hatua kwa kusaidiana na Idara ya Polisi wa Kimataifa (Interpol).
 Habari zinasema Serikali ya China imewakamata watu saba kuhusiana na pembe hizo. Tukio hilo bila shaka ni pigo kubwa kwa Serikali ya Tanzania, ikiwa ni siku chache tangu iombe upya kwa Umoja wa Mataifa kuuza akiba yake ya pembe za ndovu ili kupata fedha za kuimarisha ulinzi, hivyo kumaliza kabisa tatizo la ujangili. Ni tukio ambalo wachambuzi wa masuala ya wanyamapori wa kimataifa wanasema linaweza kuinua mboni za mamlaka za jumuiya za kimataifa na kujiuliza kama kweli Tanzania inayo dhamira ya kweli ya kukomesha ujangili.
Tuliposema mwanzoni mwa tahariri hii kwamba tukio hilo bila shaka litakuwa limewashtua na kuwakasirisha watu wengi hapa nchini, tulikuwa na maana kwamba wapo baadhi ya Watanzania ambao wamehusika kwa namna moja ama nyingine na biashara hiyo haramu na kwa sababu wametanguliza ubinafsi na kuweka kando uzalendo, wako tayari kuuza nchi yetu ili wapate utajiri.  Kitendo cha kula njama na raia wa kigeni kujenga mitandao ya kijangili katika mbuga zetu za wanyama, hakiwezi kutafsiriwa vingine isipokuwa uhaini. 
Tunapata shida kuelewa kwa nini vitendo vya ujangili vimezidi kuongezeka. Pamoja na kesi nyingi za aina hiyo kuripotiwa kupelekwa katika mahakama zetu kila kukicha na polisi kudai wana ushahidi wa kutosha dhidi ya watu hao, hivyo kuwafungulia mashtaka mahakamani, hatuoni matokeo ya kesi hizo. Kutokana na uzito wa makosa hayo, wananchi wangetegemea kesi hizo za uhaini na uhujumu uchumi siyo tu ziendeshwe kwa hati ya dharura, bali pia usiwepo uwezekano wowote wa watuhumiwa kupewa dhamana.
Tunasema hivyo kwa uchungu mkubwa kwa sababu tukio hilo la kukamatwa kwa vipande 1,209 vya pembe za ndovu zilizotoka Tanzania ni kubwa, kwani lina maana kwamba vilitokana na kuuawa kwa tembo wasiopungua 500. Hiyo siyo idadi ndogo kwa kipimo chochote kile na ni ishara kwamba Watanzania wamekosa uzalendo kwa sababu haiwezekani ujangili mkubwa kiasi hicho ufanyike pasipo kuwapo watu walioshuhudia na kuamua kukaa kimya.
Umefika wakati sasa Serikali iache kutoa machozi ya mamba kila mara matukio hayo yanapotokea. Lazima sasa vitendo vya ujangili vipewe adhabu kali kama kifungo cha miaka 30 jela au hata kifungo cha maisha, mbali na kuundwa kwa jeshi maalumu kama ilivyofanya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyounda KMKM kwa lengo la kudhibiti magendo ya karafuu. Tatizo hapa ni kutokuwapo sheria kali zinazokwenda na wakati. Hivyo, tusizilaumu mahakama kwa kutoa adhabu nyepesi kwa makosa mazito kwa sababu mahakama hizo zinafanya hivyo kwa mujibu wa sheria zilizopo. 

mwananchi

No comments:

Post a Comment