Wednesday 3 October 2012

Sumatra yakwamisha usafiri wa treni Dar

 
mwananchi

USAFIRI wa treni ya abiria uliokuwa umepangwa kuanza jijini Dar es Salaam jana umekwama kufuatia Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kutopewa leseni na kutoidhinishiwa viwango vya nauli na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Uongozi wa TRL ulisema jana kuwa, inasubiri kauli ya mwisho ya Sumatra kuhusu usafiri huo ili itoe taarifa rasmi kwa umma juu ya treni hiyo kuanza huduma ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Msemaji wa TRL, Midladjy Maez aliliambia gazeti hili jana kuwa usafiri huo unatarajiwa kuanza kazi siku yoyote kuanzia sasa, lakini mpaka Sumatra watakapotoa leseni ya usafirishaji  na kuweka viwango vya nauli.

Alisema tayari wamewasilisha mapendekezo ya viwango hivyo vya nauli na kuomba leseni ya usafirishaji Sumatra, ikiwa ni pamoja na kuitaka mamlaka hiyo ikague treni hiyo kujiridhisha na usalama wake.

“Hatuwezi kusema usafiri utaanza lini, lakini tayari kila kitu kimekamilika kwa sababu tulishapeleka Sumatra mapendekezo ya nauli na maombi ya leseni ya usafirishaji na sasa tunachosubiri ni majibu...,” alisema Maez na kuongeza;

“Tunafahamu kuwa, watu wengi wanataka kujua siku ya kuanza usafiri wa treni, ila tunaomba wasubiri maandalizi yakikamilika kila kitu kitawekwa wazi…”

Maez alifafanua kuwa usafiri huo utajumuisha mabehewa 14 ambayo kwa sasa yote yapo tayari  na kwamba kutakuwa na treni mbili zitakazokuwa na mabehewa sita kila moja, mabehewa mawili yatakuwa ya akiba.

“Tayari mabehewa 14 yamekamilika ambapo kutakuwa na treni mbili ambazo kila moja itakuwa na mabehewa sita pamoja na mabehewa mawili yatakuwa ya akiba.”

Akizungumzia ratiba ya treni hiyo, Maez alisema kuwa kutakuwa na safari mbili  kwa siku.

“Asubuhi kutakuwa na treni kutoka Ubungo Maziwa hadi mjini,  jioni treni hiyo itatoka mjini hadi Ubungo Maziwa. Vituo vya treni vitakuwa vinane na itakuwa ikibeba abiria 950 na kila behewa litapakia abiria 160.” alisema Maiz.

Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya TRL, Meneja Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema taarifa zitawekwa wazi baadaye na kusisitiza kuwa usafiri huo uko chini ya taasisi mbalimbali za Serikali.

“Taratibu za kuhakikisha treni inaanza kutoa huduma zinaendelea na taarifa rasmi itatolewa.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,  Omari Chambo alisema kuwa, pamoja na kuchelewa, usafiri huo wa treni utaanza ndani ya mwezi huu kama ilivyopangwa.

“Hatukusema kuwa usafiri utaanza Oktoba Mosi, bali tulisema utaanza mwezi Oktoba na hakuna kilichobadilika mpango huo bado upo palepale,” alifafanua Chambo.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema usafiri huo utaanza mwezi Oktoba baada ya kukamilika ukarabati wa reli kutoka Ubungo hadi Stesheni.

Alisema kufikia mwezi huu, treni hiyo itaanza kubeba abiria ili kupunguza matatizo ya usafiri kwa wakazi waishio maeneo inapopita treni hiyo.

Mabasi ya Dart
kubeba abiria 140

Wakati huohuo; aina saba za mabasi yenye uwezo wa kupakia abiria 60 hadi  140  yanatarajiwa kutumika katika mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) unaotarajiwa kuanza katika hatua ya majaribio mwezi huu.

Mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi kwa Jiji la Dar es Salaam mwaka 2014.

Dart ni mfumo mpya wa usafiri wa umma unaoanzishwa jijini hapa utakaotumia mabasi makubwa yaendayo haraka kwa kutumia njia maalumu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa Usafirishaji na Maendeleo wa Dart, Asteria Mlambo alisema; “Dira yetu ni kuwa na mfumo wa usafiri wa umma wa gharama nafuu unaowapatia faida waendeshaji.”

Alisema mabasi hayo lazima yakidhi viwango vya ubora wa huduma hususan unaozingatia uhifadhi wa mazingira na utumiaji wa njia maalumu.

Alisema mpango madhubuti wa DART ni kuboresha matumizi ya barabara ili kupunguza msongamano usio wa lazima kwa kuweka njia maalumu .

Alisema huduma bora inayopatikana katika mradi huo itachangia kuondoa au kupunguza umaskini, kuinua hali ya maisha, kuleta ukuaji wa uchumi jijini Dar es Salaam na itachochea ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi katika nyanja ya usafirishaji.
Mradi wa mwendo kasi unatarajiwa kuokoa Sh4 bilioni, ambapo utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Muungano wa Wenye Viwanda nchini (CTI) umebainisha msongamano wa magari unasababisha hasara ya asilimia 20 kwa wafanyabiashara na wafanyakazi kuchelewa kazini.
 

No comments:

Post a Comment