KAMBI YAKE YAPETA UWT, SASA WAJIPANGA UVCCM,
WAZAZI
KAMBI ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa imeendelea kuyanyanyasa makundi mengine ndani ya CCM, ambayo
yamekuwa yakijipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kambi ya kiongozi huyo ni kama imehamia
Dodoma ili kuhakikisha watu wake wanashinda katika chaguzi za viongozi
wa juu wa jumuiya za CCM baada ya kufanikisha kile inachodai kuwa
ushindi mkubwa katika ngazi za wilaya na mkoa kutokana na watu wake
wengi kushinda.
Wapambe wa Lowassa wakiongozwa na
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja
wa Vijana (UVCCM), Hussein Bashe wapo Dodoma kabla ya kuanza kwa
Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) na wataendelea
kuwapo mpaka jumuiya zote zitakapokuwa zimefanya uchaguzi huo.
“Hapa kazi ni moja tu, hakuna kulala
maana tukilala tutajikuta tumewekwa pabaya. Tumefanikiwa UWT na sasa
tunaelekeza majeshi yetu UVCCM... lazima tuhakikishe tunakomesha uonevu
wa kuitana magamba mwaka huu,” alisema mmoja wa wapambe wa Lowassa juzi
usiku.
Matokeo ya uongozi wa juu wa UWT
yameongeza matumaini kwa kambi hiyo ambayo imezoa zaidi ya asilimia 80
ya viongozi katika jumuiya hiyo yenye ushawishi mkubwa katika uamuzi
mbalimbali wa chama hicho.
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba
ambaye alitetea vizuri nafasi yake na Makamu wake, Asha Bakari Makame
wanatajwa kuwa katika kambi hiyo huku wajumbe saba kati ya tisa
waliochaguliwa kuiwakilisha jumuiya hiyo katika Halmashauri Kuu ya Taifa
(Nec) ya chama hicho, wakiwa waumini wa kambo hiyo.
Walioshinda nafasi za ujumbe wa NEC
ambao wanatajwa kuwa wafuasi wa Lowassa ni pamoja na Mbunge wa Ukonga,
Eugen Mwaiposa, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Shamsa
Mwangunga na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
Pindi Chana.
Wengine ni wabunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo, Zainabu Kawawa, Mary
Mwanjelwa na Subira Mgalu.
Wajumbe wawili ambao ni pamoja na Naibu
Waziri wa Fedha, Janeth Mbene yeye anatajwa kuwa hana kundi lolote
wakati Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu ambaye anatajwa kwamba
alikuwa akimuunga mkono Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela.
Kilango ambaye alikuwa akiungwa mkono na makundi ya watu waliojipambanua
kuwa wapambanaji na ufisadi, aliangushwa vibaya na Simba kwa zaidi ya
kura 400 katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa UWT.
Vigogo wengine wanaotajwa kuwa na kambi
katika kinyang’anyiro hicho cha urais wa 2015 ni Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambao katika uchaguzi wa jumuiya za CCM
nguvu zao zinaonekana kuwa si kubwa kama ilivyotarajiwa.
JK awapasha viongozi UWT
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete juzi usiku aliwatolea uvivu
viongozi wa UWT, akiwataka kuchukua hatua za kumaliza nyufa
zilizosababishwa na uchaguzi uliomalizika Jumamosi iliyopita.
Rais Kikwete alisema viongozi
waliochaguliwa wakiongozwa na Simba ambaye pia Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto wachukue hatua kuondoa makundi ambayo yanatokana
na uchaguzi.
“Hii jumuiya siyo yenu, ni ya wanachama
kwa hiyo baada ya uchaguzi lazima muwe tayari kufanya kazi na kila
mmoja, isije ikawa ni wale marafiki zako tu maana ikiwa hivyo utamteua
hata kama uwezo hana,” alisema Kikwete alipokuwa akifunga mkutano huo wa
uchaguzi mjini Dodoma.
Alikemea tabia ya chuki inayojengwa na
uchaguzi akisema inatokana na viongozi walioko katika nafasi mbalimbali
za uongozi kudhani kwamba wanazimiliki binafsi.
“Hupaswi kumchukia mtu eti kwa sababu
amegombea nafasi fulani, hakuna nafasi ya mtu, nafasi zote ni za chama,
kwa hiyo kama ulikuwa mwenyekiti, uongozi wako unakoma pale
tunapotangaza upya uchaguzi,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tukishatangaza kila mwanachama mwenye sifa anakuwa na haki ya kugombea
nafasi hizo, sasa wewe usimchukie na kumuuliza eti kwa nini unagombea
nafasi yangu, siyo nafasi yako, hii ni nafasi ya chama.”
Alikemea tabia ya baadhi ya viongozi au
wagombea kuwajengea chuki wale ambao hawakuwaunga mkono, na kwamba
anayefanya hivyo hapaswi kuwa kiongozi.
Alisema kiongozi wa aina hiyo daima ataongoza kwa makundi, akiwapenda
wale waliomuunga mkono na kuwatenga wale ambao walikuwa na mtazamo
tofauti jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa jumuiya na chama kwa jumla.
“Kila mwanachama ana uhuru wa kumuunga
mkono mtu anayempenda, sasa wewe unapomkasirikia na kumjengea chuki
unamaanisha nini? Demokrasia maana yake ni kila mmoja wetu kumchagua mtu
anayeona anafaa,” alisema.
Alitoa mfano kwamba baada ya yeye
kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM mwaka 2005 na baada ya
uchaguzi uliompa ushindi, aliwateua wale waliokuwa washindani wake
katika Baraza la Mawaziri, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
“Mwandosya tuko naye hadi leo, hata
wale waliokuwa wakinipinga na wengine walinifanyia mambo ya ajabu
kwelikweli, lakini hayo yote inafika mahali unaweka kando maana huwezi
kuongoza nchi kwa kuwateua marafiki zako tu,” alisema Kikwete.
No comments:
Post a Comment