Tuesday, 2 October 2012

WOLPER AWATAJA WALIOVUNJA UCHUMBA WAKE NA DALLAS


Na Mwandishi Wetu
SIYO habari mpya kwamba ule uchumba wa kitajiri kati ya staa wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper Massawe na mfanyabiashara ‘mjanjamjanja’, Abdallah Mtoro ‘Dallas’ umevunjika, kinachotengeneza kichwa cha habari leo ni sababu iliyo nyuma ya kuachana kwao.
Uwazi ‘Mama wa Magazeti Pendwa’, linakuwa la kwanza kuanika sababu ya kuachana kwao, ikiwa ni kutaja majina ya watu ambao wamekuwa sababu ya kumwagana kwao.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, sababu ya kwanza ni Wolper kuwa na hisia mbaya dhidi ya wanawake kadhaa, akiamini kwamba kuna kitu cha zaidi kati yao na Dallas.
Chanzo chetu kikataja majina ya watuhumiwa: “Lulu Mathias Semagongo ‘Aunty Lulu’, Halima Haroun ‘Halima Kimwana Manywele’, Khadija Shaibu ‘Dida’, Mohamed Ndama ‘Mtoto wa Ng’ombe’ na mwanamke mwengine aliyetajwa kwa jina moja la Sabaha.”
Kikafafanua sababu ya kila mmoja kutajwa: “Dida anatajwa kwa sababu moja kuu, kwa muda mrefu amekuwa akitambulika kama dada wa Dallas, kwa hiyo akawa anamwita Wolper wifi. Baadaye Wolper akawa na hisia mbaya na Dida, akaanza maswali.
“Kwa kawaida Dallas ni mtu asiyejali, kwa hiyo akawa anampotezea, yaani hampi majibu yaliyonyooka. Wolper alikuwa anataka kujua Dida ni dada yake Dallas kivipi? Kimjinimjini au ni ndugu kabisa. Wolper alipoona hakuna jibu la kunyooka, akaweka kinyongo, akawa hana imani na Dida.
“Wolper anaamini kwamba Dallas ametembea na Aunty Lulu, Halima Kimwana na Sabaha. Upande wa Ndama, Wolper alishamshtaki Ndama kwa kumtapeli. Sasa hivi Dallas na Ndama wapo pamoja, kwa hiyo Wolper anahisi anasalitiwa na mchumba wake. Mwisho akaona bora waachane.”
Baada ya maelezo hayo kutoka kwa chanzo chetu, mwandishi wetu alizungumza na Wolper ambaye alikiri kuachana na Dallas, alipobanwa kuhusu sababu alikata simu, baadaye akaandika SMS: “Dallas ni mchafu, nimeshamfumania sana. Anatembea na wanawake hovyo.”
Alipopigiwa simu mara ya pili na kutakiwa kutaja majina ya wanawake ambao ameona wamekuwa na uhusiano na Dallas, hakuyaweka wazi ila alisema: “Nikiwazungumzia nitaonekana namuonea wivu, ila kwa kifupi Dallas amenidhalilisha. Ametembea mpaka na wanawake ambao siyo daraja langu kabisa.
“Mimi nilimheshimu Dallas, unajua alipokuwa nje alikuwa ananiheshimu kama mke wake mtarajiwa. Unajua mtu tabia yake utaijua mkiwa pamoja. Sasa aliporudi hapa na vitendo alivyofanya ndiyo nimeamini siyo mtu mzuri, hastahili kuwa mume wangu kabisa.
“Wakati mwingine nimekaa nyumbani, naambiwa Dallas yupo na wanawake. Navaa kininja, nakodi teksi, nikifika nashuhudia kila kitu halafu narudi nyumbani. Nimejionea mengi na mpaka sasa simhitaji tena. Nimeona wanawake zake, siyo hadhi yangu lakini kanichanganya nao.”
Aunty Lulu alipoulizwa alisema, hajawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dallas, akaongeza: “Tatizo Dallas anapenda sana utani, unaweza kukaa naye, watu wakija ananitambulisha mimi ni mke wake. Hilo ndiyo tatizo.”
Dida yeye alisema anashangaa kutajwa kwenye sakata la Wolper na Dallas kwa sababu ana zaidi ya miaka saba, hajakutana na mfanyabiashara huyo mjanjamjanja.
Halima Kimwana, Ndama na Dallas hawakupatikana lakini nafasi yao bado ipo ili nao waelezee kilichopo upande wao. Waandishi wetu bado wapo kazini wanawatafuta.

gpl

1 comment:

  1. Wolper mm niko tayari kwa ku kuowa!!!!!!

    ReplyDelete